1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume mpya ya Samia yazua mjadala Tanzania

19 Mei 2026

Rais Samia Suluhu Hassan ameunda tume ya uchunguzi wa jinai kuhusu matukio ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29. Hatua hiyo imezua mjadala mkubwa huku upinzani na wanaharakati wakionesha wasiwasi kuhusu uwazi wake.

https://p.dw.com/p/5DyI7
Tanzania 2026 | Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Ikulu Dar es Salaam
Rais Samia alitangaza kuundwa kwa tume ya uchunguzi wa jinai kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Othman Chande, ili kubaini waliohusika hasa na uharibifu na mauaji ya Oktoba 29.Picha: State House of Tanzania

Mjadala unaendelea nchini Tanzania baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kuundwa kwa tume ya uchunguzi wa jinai kuhusu matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29. Hatua hiyo imepokelewa kwa mitazamo tofauti kutoka kwa vyama vya siasa, wanaharakati na wananchi wa kawaida. Wakati baadhi wakiiona ni hatua ya kutafuta ukweli, wengine wanaonyesha mashaka kuhusu uwazi wake.

Tume hiyo imeundwa kufuatia mapendekezo ya tume iliyokuwa chini ya Jaji Chande, iliyochunguza matukio ya uchaguzi mkuu. Hata hivyo, ripoti ya tume hiyo bado haijawekwa wazi kwa umma. Jambo hilo limekuwa moja ya sababu kuu zinazotajwa na wakosoaji wa hatua hiyo mpya.

Kupitia taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, serikali ilisema tume hiyo mpya itaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shabani Ally Lila. Wajumbe wengine watatu ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Serikali inaeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha matukio yote yanayolalamikiwa yanachunguzwa kwa kina.

Vyama vya upinzani na watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakieleza wasiwasi kuhusu mazingira ya kuundwa kwa tume hiyo. Wanasema ni vigumu kuamini mchakato ambao msingi wake haujawekwa wazi kwa wananchi. Pia wanahoji kwa nini ripoti ya Jaji Chande bado haijachapishwa rasmi.

Tanzania 2026 | Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, Jaji Mohamed Chande Othman akiwasilisha Ripoti ya Uchunguzi wao kwa Rais Samia Suluhu Hassan mbele ya hadhira.
Miongoni mwa mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande (anaezungumza pichani), ni kuundwa kwa tume maalumu ya kubaini wahusika wakuu wa vurugu za Oktoba 29.Picha: Tanzania state House 

Mkurugenzi wa mambo ya nje wa chama cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo, John Kitoko, alisema chama chake kina mashaka na tume hiyo mpya. “Kwanza ripoti yenyewe haijawekwa hadharani, hatujui kilichomo ndani ya ripoti. Kilichosomwa na Jaji Chande ni hotuba tu ya kukabidhi ripoti hiyo, hivyo ni vigumu kusema kwa uhakika kwamba hiyo ndiyo taswira halisi ya ripoti,” alisema Kitoko.

Upinzani waendelea kuhoji uwazi wa tume

Baadhi ya wachambuzi wanaamini kazi inayotarajiwa kufanywa na tume mpya ingeweza kukamilishwa na tume ya Jaji Chande. Kwa maoni yao, serikali ilipaswa kuanza kwa kutoa taarifa kamili kwa umma kabla ya kuunda chombo kingine cha uchunguzi. Hali hiyo imeongeza mijadala kuhusu matumizi ya fedha za umma na ufanisi wa tume hizo.

Watetezi wa haki za binadamu pia wameonyesha wasiwasi kuhusu uhuru wa tume hiyo mpya. Wanasema wananchi wanahitaji kuona hatua za kweli za uwajibikaji na si kuongeza tume nyingine bila matokeo yanayoonekana. Kwao, suala kubwa ni haki kwa waathirika wa matukio ya uchaguzi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, LHRC, Anna Henga, alisema tume hiyo mpya inaweza kuongeza urasimu badala ya kutoa suluhisho. “Kwa sababu tume hizo zinatumia kodi zetu, bado tunaona kazi inakuwa mara mbili au tatu zaidi. Tume yenyewe haiwezi kumkamata mtu, itabidi iwaagize polisi kufanya hivyo,” alisema Henga.

Marufuku kuripoti ushuhuda wa waathiriwa wa ghasia Tanzania

Wakosoaji wengine wanaona hatua hiyo inaweza kuchelewesha juhudi za kutafuta suluhu ya kisiasa. Wanasema badala ya kuongeza tume mpya, viongozi wanapaswa kuwekeza nguvu katika maridhiano ya kitaifa. Kwa upande wao, wanaamini mazungumzo ya kisiasa yanaweza kusaidia zaidi kurejesha imani ya wananchi.

Licha ya ukosoaji huo, baadhi ya wananchi wameonyesha matumaini kuhusu tume hiyo mpya. Wanasema kuundwa kwake kunaweza kusaidia kuweka wazi yaliyojiri wakati wa uchaguzi mkuu. Pia wanaamini hatua hiyo inaweza kufungua njia ya kuwawajibisha waliohusika na vitendo vya ukiukwaji wa sheria.

Wapo wanaoona ni hatua ya mbele

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanaamini hatua ya Rais Samia ni ishara ya nia ya kutafuta ukweli. Wanasema tume hiyo inaweza kusaidia kupunguza mvutano wa kisiasa uliotokea baada ya uchaguzi. Aidha, inaweza kuwa mwanzo wa mjadala mpana kuhusu mageuzi ya uchaguzi nchini Tanzania.

Bob Yona, ambaye amekuwa akifuatilia hali ya kisiasa nchini kwa muda mrefu, alisema tume hiyo inaweza kusaidia kubaini wahusika wa matukio yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi. “Wahusika mbalimbali ambao walitekeleza uhalifu huo ndani ya serikali na nje ya serikali vilevile, tusubiri kidogo tuone jinsi gani tume itafanya tathmini yake,” alisema Yona.

Wapo pia wanaoamini kuwa kuundwa kwa tume hiyo kunaweza kuonyesha serikali ipo tayari kusikiliza malalamiko ya wananchi. Hata hivyo, wanasema mafanikio yake yatategemea uwazi wa kazi yake na namna matokeo yatakavyowasilishwa kwa umma. Bila uwazi, wanaonya kuwa wananchi wataendelea kuwa na mashaka.

Rais Samia atoa wito wa mshikamano wa kitaifa

Kwa sasa bado haijafahamika ni lini tume hiyo itaanza kazi rasmi. Serikalipia haijaeleza muda ambao tume hiyo itatumia kukamilisha uchunguzi wake. Hilo limeendelea kuongeza maswali kutoka kwa wananchi na makundi ya kijamii.

Kadri mjadala unavyoendelea, suala kubwa linalobaki ni iwapo tume hiyo itaweza kujenga imani ya wananchi na kuleta ukweli unaotarajiwa. Wengine wanaiona kama nafasi ya uwajibikaji, huku wengine wakihofia inaweza kuwa mchakato mwingine usioleta mabadiliko makubwa. Hata hivyo, wengi wanakubaliana kuwa taifa linahitaji majibu ya wazi kuhusu yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu.