Je, unafahamu kwamba nyenje ni chanzo cha protini?

Je, unafahamu kwamba nyenje ni chanzo cha protini?
Katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, kutokana na ufadhili wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kundi la vijana wanajishughulisha na ufugaji wa wadudu nyenje (Crickets) ili kukabiliana na changamoto ya utapiamlo miongoni mwa watoto wachanga. Anold Kayanda na maelezo zaidi.
Video iliyorekodiwa na WFP katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma kaskazinimagharibi mwa kaunti ya Turkana nchini Kenya inaonesha vijana wakionja wadudu hawa nyenje.
Nyenje, wadudu wanaoelekea kufanana na panzi lakini wao hutoa sauti ya mlio mkali hususani nyakati za usiku, kumbe ni chakula kitamu kilichothibitika kuwa suluhisho endelevu la lishe.
Gloire Lukambo, mwanachama wa kikundi cha Vijana Twaweza humo kambini Kakuma anasema, “Kufuga nyenje kunatupa virutubisho vingi, hasa protini ambazo samaki wanahitaji ili kukua vizuri, lakini kwa muda tumejifunza kuwa ni chanzo kizuri cha protini kwa watoto, hasa watoto wachanga.”

WFP ilisaidia kundi hili la vijana wakapata mafunzo kuhusu ufugaji wa wadudu katika moja ya vyuo vikuu nchini Kenya. Wanawafuga katika makasha madogo madogo ya mbao, ndani wameweka trei za kubebea mayai ya kuku. Zaidi ya faida ya lishe, Gloire Lukambo kuna faida nyingine za ufugaji wadudu hawa aina ya nyenje.
Gloire anasema, "yote haya pia yanakuwa pia faida ya kifedha. Ufugaji wadudu hauna athari kubwa kwa mazingira. Haichukui muda mwingi kufuga wadudu."