Nitamuita mtoto wangu Amani kwasababu amezaliwa katika vita, DRC

Nitamuita mtoto wangu Amani kwasababu amezaliwa katika vita, DRC
Wakati mapigano yalipozidi kushika kasi katika Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), Francine Toyata alishikilia tumbo lake la ujauzito, maumivu yakimshika kwa wimbi la uchungu. Ilikuwa saa 2 asubuhi wakati alipoanza kusikia uchungu wa kujifungua, katikati ya eneo la vita. "Nimehamishwa mara mbili tangu Januari, na nilikuwa nikijificha katika kambi iliyojaa watu kupita kiasi," ameliambia shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu (UNFPA).
Mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa kundi la Mouvement du 23 Mars (M23) yalizuka mnamo Januari 2025 karibu na Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini. Mamia ya maelfu ya watu walilazimika kukimbia kutoka nyumbani na kutafuta hifadhi katika kambi rasmi na zisizo rasmi, katika eneo ambalo tayari lilikuwa na msongamano mkubwa wa watu waliokimbia makazi yao.

Bi. Toyata anatokea Kabati, katika wilaya ya Rutshuru, lakini alikimbia na mumewe mwezi Februari 2023 wakati mapigano yalipozidi kushika kasi katika eneo lao. Sasa, huku sauti za mabomu zikisikika kambini, alisafiri kwa giza na machafuko pamoja na mama yake kufika kwenye kliniki ya afya ya kuhamahama ya UNFPA na kufika kwa wakati.
Upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi za kuokoa maisha ulikuwa adimu katika eneo hilo hata kabla ya kuzuka kwa mapigano ya sasa, na nchi hiyo ilikuwa na viwango vya juu zaidi duniani vya vifo vya akina mama kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito na kujifungua.
Sasa, wakati hospitali moja tu kati ya tatu katika eneo hilo na kituo kimoja kati ya vitano vya afya vinavyoweza kufanya kazi, timu za kliniki za afya za kuhamahama za UNFPA mara nyingi ndio chaguo pekee wanawake wanalo kwa ajili ya kujifungua na msaada wa wataalamu wa afya.
Muda wa saa mbili baada ya kufika, Bi. Toyata alijifungua mtoto wa kike salama.Lakini katika hali hatari zaidi. Akiangalia mtoto wake wa kike, anasema, "nitamuita amani. Kwa sababu alizaliwa katika vita, lakini atasimama kwa ajili ya amani."

Hatari Nyingi kwa Wanawake na Wasichana
Licha ya kuwa ni mojawapo ya maeneo machache yaliyobaki salama kwa wanawake na wasichana waliokimbia makazi yao katika Kivu Kaskazini, hema dhaifu linalohifadhi kitengo cha afya cha kuhamahama limetoa ulinzi mdogo dhidi ya milipuko inayokaribia.
"Ni kwa wanawake kama Francine ndiyo tunafanya kazi hii. Hatukuwa salama. Tunahitaji msaada zaidi ili kukutana na mahitaji haya ya haraka." Anasema mkunga wake, Nelly.
Kati ya wanawake 220,000 waliokadiriwa kuwa na ujauzito katika Kivu Kaskazini na Kivu Kusini pekee, zaidi ya 12,000 kwa sasa wamefurushwa, na hawana uhakika wa kupata huduma za matibabu. Zaidi ya wanawake na wasichana 88,000 wako katika hatari ya kuwaathiriwa na vitendo vya vurugu za kijinsia, na ujauzito usio wa kupangwa,unatarajiwa kuongezeka kutokana na kuanguka kwa huduma za afya.
Katika miaka ya karibuni, matukio ya vurugu za kijinsia, ikiwemo mashambulizi, ubakaji na ulazimishaji, yameongezeka sana nchini kote, na matukio mawili kati ya tatu yakiripotiwa katika mikoa ya mashariki ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini. Ukosefu wa usalama katika kambi zilizozidiwa na wakimbizi, njaa na kukosekana kwa fursa za kupata kipato cha uhakika pia kumewaacha wengi na maeneo machache ya kutafuta msaada kwa familia zao. Hatari za unyanyasaj na matumizi mabaya kwa wanawake na wasichana vijana, ikiwa ni pamoja na ndoa za kulazimishwa, biashara ya usafirishaji haramu ya binadamu na unyanyasaji wa ngono, inaripotiwa kuongezeka kwa kasi pia.
Upatikanaji wa Huduma za Afya ya Uzazi Zilizoshindikana

Hii ni pamoja na kupunguzwa kwa upatikanaji wa huduma za afya ya kijinsia na uzazi kutokana na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na kupungua kwa rasilimali, huku njia muhimu za kibinadamu zikifungwa na mapigano.
Kadri vita vinavyoendelea, mabomu yameanza kugonga kambi za wakimbizi wa ndani, na kulazimisha wanawake na wasichana wengi kukimbia tena, na kuwaondolea kabisa hifadhi walizokuwa nazo. Baadhi ya kliniki za afya za kuhamahama za UNFPA na vituo vya kusikiliza pia vimevamiwa, kuharibiwa na kusitisha huduma kwa muda, na kupunguza zaidi chaguzi zilizokuwa zinapatikana kwa watu waliokuwa na mahitaji makubwa.
Mahitaji muhimu ya haraka
UNFPA kwa sasa inafanya kazi na kliniki nane za afya za kuhamahama katika eneo hilo, ambazo zina wahudumu 27 wa uzazi wakitoa huduma muhimu za uzazi na afya ya uzazi. Vituo vitatu vya afya vinavyohudumia wakimbizi katika kambi nane vina hakikisha wajawazito wanajifungua salama, huduma za uzazi kabla ya kujifungua, na upangaji uzazi kwa zaidi ya watu 8,000.

Vidonge vya uzazi na rasilimali nyingine za afya ya uzazi zinagawiwa, licha ya hali hatarishi na usumbufu. Kwa waathirika na wale walio katika hatari ya vurugu za kijinsia, huduma za dharura zinapeana msaada wa haraka, miongozo, na ulinzi chaguzi huku maeneo matano yaliyoungwa mkono na UNFPA kwa wanawake na wasichana yakiendelea kutoa hifadhi na msaada wa kisaikolojia.
UNFPA inaendelea kuwa Kivu Kaskazini, ikifanya kazi kwa pamoja na serikali na washirika wa kibinadamu kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma za kuokoa maisha. Lakini mahitaji yanaongezeka kwa kasi kuliko rasilimali zinazoweza kufikiwa. Simulizi ya Francine siyo ya kipekee. Kuna maelfu ya wanawake wengine wanaojitayarisha kujifungua katika mahema, chini ya mashambulizi, bila uhakika kama wao au watoto wao wataweza kuishi usiku.