Redio ya TBC Taifa yaenda na wakati kuelimisha kuhusu tabianchi

Redio ya TBC Taifa yaenda na wakati kuelimisha kuhusu tabianchi
Katika maadhimisho ya siku ya redio duniani, Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imefahamu jinsi redio mshirika wake, TBC Taifa ambayo ni ya shirika la Utangazaji Tanzania, TBC inatumia kituo hicho kinachosikika takribani asilimia 92 ya eneo la taifa hilo la Afrika Mashariki, kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, lilichagua maudhui ya siku hii kuwa Redio na Mabadiliko ya Tabianchi ambapo linasema lengo ni kudhihirisha jukumu la redio katika kusambaza ujumbe na kuelimisha kuhusu changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kutanabaisha kuhusu hatua endelevu na kuwapa sauti wanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi.
Na katika kuchambua maudhui hayo Assumpta Massoi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa amezungumza na Teonas Aswile, Mtangazaji na Mtozi wa kipindi cha Urithi Wetu kinachomulika masuala ya mazingira ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.
Bwana Aswile amekuwa akiandaa kipindi hicho kwa miaka 6 sasa na alipoulizwa ni kwa vipi anajumuisha mabadiliko ya tabianchi kwenye Urithi Wetu akasema, “huwa nakaribisha wataalamu kuchambua mada mbalimbali na pia ninatumia waandishi wa habari wa TBC walioko mikoani.”
Kupitia redio wananchi wanalinganisha hali ya sasa na zamani
Amesema anashirikisha pia wadau wa TBC walioko Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar akiwauliza, “mazingira yao siku za nyuma yalikuwa vipi ikilinganishwa na sasa? Tabia ya baharí au maziwa na mito iko vipi hivi sasa. Ardhi iko vipi? Upatikanaji wa vitoweo kama samaki sasa na zamani ni vipi?”
Anashirikisha msikilizaji kwa njia ya simu ambapo wanatuma ujumbe mfupi kupitia njia ya simu ya kiganjani na msikilizaji anaweza kuzungumza moja kwa moja hewani kupitia simu ya mezani iliyounganishwa studio.
Wataalamu na mchango wao kupitia redio
Lakini vipi wanaharakati wa mazingira kama ambavyo UNESCO inasema wapatiwe sauti? Bwana Aswile akasema hilo linafanyika na alimkaribisha studioni Walter Yobu, mwanamazingira, mtafiti na mwandishi wa vitabu.
Bwana Yobu alitumia fursa hiyo kuainisha maana ya tabianchi akisema ni “mwenendo wa hali ya hewa, yakiwemo majira, mtawanyiko wa mawingo, viwango vya mvua, theluji pamoja na upepo. Na tunapozungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi, tunamaanisha ni mabadiliko ya dunia yanayosababishwa na ongezeko la miali ya jua baada ya kuharibiwa au kuathiriwa tabaka la juu la anga.”
Redio ni moyo wa habari
Mtangazaji akamuuliza mtaalamu iwapo redio bado ina nafasi ya kufikisha ujumbe zama hizi za maendeleo ya teknolojia, mtaalamu akasema nafasi bado ni kubwa sana kwa kuwa redio ina uwezo wa kufikia watu wengi kwa wakati mmoja tena kwa urahisi.
“Umoja wa Mataifa kupitia UNESCO iwezeshe redio kufanya kazi yake kwa kuzingatia ni mahali panapikwa taarifa muhimu,” amesema Bwana Yobu.
Vijana wa bofya, tazama, soma, funga
Maendeleo ya teknolojia yanaonekana penginepo kusababisha watu kuipa redio kisogo. Bwana Aswile kwa kutambua hilo, na zaidi kwamba vijana wengi wako kwenye teknolojia zaidi akanieleza kile anachofanya.
“TEHAMA tunaitumia chanya na hasa kwenye kuwashirikisha umma ambao unatufuatilia. Fahamu kwamba kuibuka kwa mitandao ya kijamii kumeleta changamoto kubwa sana. Vijana wamehamia kwenye mitandao ya kijamii. Na mimi nawaita hawa ni vijana wa bofya, tazama kilichopo, funga ondoka. Hivyo sisi tunatuma taarifa zetu na mada zetu kwenye mitandao ya kijamii, na kisha kuwapatia fursa ya kutoa maoni, maoni ambayo tunasoma kwenye kipindi cha Urithi Wetu.”