Wakiingia Bukavu, M23 wameua watoto na kukiuka haki za binadamu- OHCHR

Wakiingia Bukavu, M23 wameua watoto na kukiuka haki za binadamu- OHCHR
Hali ya haki za binadamu Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, inaendelea kuzorota kwa kasi, na kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na unyanyasaji,ukatili kama vile watu kuuawa kiholela, wakiwemo watoto, na mizozo inayohusiana na unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji wa kijinsia, amesema Ravina Shamdasani Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu OHCHR.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko jiini Geneva, Uswisi, Bi. Shamdasani amesema, kumekuwepo na mashambulizi dhidi ya hospitali na maghala yenye shehena za misaada ya kibinadamu, pamoja na vitisho dhidi ya utawala wa mahakama.
“Mashambulio yanayofanywa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, kuelekea jimbo la Kivu Kusini yamezidisha mgogoro wa usalama na kibinadamu katika ukanda wa Maziwa Makuu na kusababisha wimbi la watu kuhama.
Bi.Shamdasani anasema ofisi yao imethibitisha visa matukio ya M23 kuua watoto kiholela mara baada ya kuingia mji wa Bukavu wiki iliyopita.
“Pia tunajua kuwa watoto walikuwa na silaha. Tunawaomba Rwanda na M23 kuhakikisha kuwa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu zinaheshimiwa. Pia tumesajili matukio ya unyanyasaji wa kingono, unyanyasaji wa kijinsia unaohusiana na mizozo, kulazimishwa kushiriki katika vita hivyo, kuogopeshwa na vitisho vya kifo,” amesema Afisa huyo wa OHCHR.
Zaidi ya hayo, amesema wamepokea taarifa kuhusu kukamatwa kiholela na vifungo, matendo ya kudhalilisha na madai ya kurudishwa kwa nguvu kwa vijana wa DRC waliokuwa wakikimbia mizozo katika nchi jirani.
Vitisho kutoka wa wafungwa waliotoroka gerezani
Kufuatia tukio la kutoroka kwa wafungwa kutoka gereza la Kabare na Bukavu kuu tarehe 14 Februari, “tumepokea maombi ya ulinzi kutoka kwa waathirika na mashahidi. Wanahofia kisasi kutoka kwa wafungwa waliotoroka , kutokana na ushiriki wao katika kesi dhidi ya baadhi ya wafungwa hawa waliokutwa na hatia za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na unyanyasaji, baadhi yake yakihusisha uhalifu wa kimataifa. Pia tuna wasiwasi kuhusu usalama wa mawakili na wafanyakazi wa kisheria.” Amesema Bi. Shamdasani.
Ukandamizaji dhidi ya wanahabari na watetezi wa haki za binadamu
Ofisi hiyo pia imepokea ripoti za wanahabari, watetezi wa haki za binadamu na wanachama wa mashirika ya kiraia kukabiliwa na viisho, na kulazimishwa kuondoka katika eneo hilo.
“Wengine bado wanakwama Bukavu na Goma, na wameeleza hofu yao kwa usalama wao, kutokana na ushiriki wao mkubwa katika haki za binadamu, na kuonesha dhihaka ya ukiukaji na unyanyasaji uliofanywa na Rwanda na M23 katika maeneo mbalimbali ya mashariki ya DRC,” amesema afisa huyo.
Yanayoendelea jimboni Kivu Kusini na Kivu Kaskazini yanatisha
Bi. Shamdasani amemnukuu Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Volker Türk, akiisihi Rwanda na M23 kulinda watu wote katika maeneo chini ya udhibiti wao
“Anasikitika kuwa matukio yanayoendelea jimboni Kivu Kusini na Kivu Kaskazini, na athari hasi kwa raia. Ukatili lazima utokomezwe mara moja. Pande zote lazima ziheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, hususan kuhusu ulinzi wa raia na sheria za haki za binadamu, na kurejea kwenye mazungumzo ya amani kupitia michakato ya Luanda na Nairobi