Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano wa kimataifa ni nini, na kwanini ni muhimu kwetu?

Bendera za Nchi Wanachama zikipandishwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York
UN Photo/Manuel Elías
Bendera za Nchi Wanachama zikipandishwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York

Ushirikiano wa kimataifa ni nini, na kwanini ni muhimu kwetu?

Amani na Usalama

'Multilateralism' yaani Ushirikiano wa kimataifa  ni neno linalotumika mara nyingi katika Umoja wa Mataifa, lakini si dhana ambayo inafaa tu kwa mikutano ambapo diplomasia ya kimataifa hufanyika.

Zaidi ya Umoja wa Mataifa, 'Multilateralism' inaathiri maisha ya kila siku ya watu kwa njia nyingi. Inasaidia kupunguza migogoro, kukuza uchumi wetu, na kuturuhusu kusafiri kwa usalama kote ulimwenguni. Pia ni muhimu katika kushughulikia matatizo makubwa ya kimataifa kama mabadiliko ya tabianchi na Akili Mnemba (AI) isiyodhibitiwa.

Maana halisi ya ushirikiano wa kimataifa

Kiasili, 'Multilateral' lilikuwa neno la hisabati za maumbo ya jiometri linalomaanisha "pande nyingi." Sasa, linatumiwa kuelezea siasa za kimataifa na diplomasia, ambapo nchi nyingi zenye mitazamo na malengo tofauti hufanya kazi pamoja.

Philemon Yang (kwenye jukwaa na kwenye skrini), Rais wa kikao cha sabini na tisa cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, akihutubia ufunguzi wa Mkutano wa Zama Zijazo tarehe 22 Septemba 2024.
UN Photo/Loey Felipe

Mfumo wa Umoja wa Mataifa ni jukwaa kuu la kimataifa ambapo nchi huungana kutatua matatizo ya kimataifa. Wanashiriki mikutano, mikusanyiko, na vikao ili kushughulikia masuala muhimu.

Ushirikiano, Maelewano, na Uratibu

Katika masuala ya kimataifa, nchi hufanya kazi pamoja (kwa ushirikiano), kufanya makubaliano (maelewano), na kupanga jitihada zao (uratibu) kutatua matatizo ambayo nchi moja pekee haiwezi kushughulikia. Hizi “C” 3 (Cooperation, Compromise, and Coordination)  husaidia kujenga imani na kutatua migogoro kwa amani.

Kufanya ulimwengu wa kisasa uwezekane

Fikiria kama kila nchi ingetengeneza mfumo wake wa kupiga simu, mashirika ya  ndege, usafirishaji au posta  na isingeshirikiana na nchi  zingine. Usafiri wa kimataifa, mawasiliano, na biashara ingekuwa katika hali ya machafuko. Shukrani kwa Ushirikiano wa kimataifa, tunayo mifumo ya kimataifa inayowezesha mambo haya kutokea.

Multilateralism huwezesha uratibu wa kimataifa katika sekta zote, ikiwa ni pamoja na mawasiliano.
© Unsplash/Brunno Tozzo
Multilateralism huwezesha uratibu wa kimataifa katika sekta zote, ikiwa ni pamoja na mawasiliano.

Ukweli kwamba tunavyo viwango vya kimataifa kwa shughuli mbalimbali za kila siku kutoka afya hadi mifumo ya posta hadi usafiri ni shukrani kwa Ushirikiano wa kimataifa, na kuundwa kwa mashirika kadhaa ya kimataifa, mengi yakiwa yameanzishwa katika karne ya 19, na sasa ni sehemu ya Mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Mashirika mawili ya kimataifa ambayo yalikuwepo kabla ya Umoja wa Mataifa ni:

Shrika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano  (ITU): Liliazishwa mnamo mwaka 1865 ili kutanua mitandao ya 'telegraph'. Sasa, husaidia katika uendeshaji wa   masafa ya redio, satelaiti, na mtandao wa intaneti.

Shirika la Umoja wa  Mataifa la Kazi Duniani (ILO): Liliazishwa mnamo mwaka 1919 ili kukuza haki za wafanyakazi, kuhamasisha fursa nzuri za ajira, kuboresha ulinzi wa kijamii na kuimarisha mazungumzo kuhusu masuala ya kazi.

Kutengeneza Sera za Kimataifa

Tangu mwaka 1945, Umoja wa Mataifa umesaidia nchi kufanya kazi  kwa pamoja na kuunda makubaliano muhimu. Kiungo cha sera cha Umoja wa Mataifa ni Mkutano Mkuu, jukwaa la kipekee kwa mijadala ya kimataifa kuhusu masuala ya kimataifa. Katika nchi 193 za Umoja wa Mataifa kila moja ina kura sawa, bila kujali ukubwa wa uchumi wao, idadi ya watu, au nguvu ya kijeshi: Kura ya Monaco ina uzito sawa na ya China.

Mafanikio ya Umoja wa Mataifa

Sifa nyingine ya Ushirikiano wa kimataifa  ni kuweka viwango. Mkutano Mkuu una jukumu hili la kimataifa na umeunda sheria nyingi za kimataifa na mikataba kuhusu kupunguza silaha, haki za binadamu, na ulinzi wa mazingira.

Watoto wakisoma tamko la haki za binadamu
UN
Watoto wakisoma tamko la haki za binadamu

Moja ya mafanikio yake makubwa ni kuandaa na kupitisha Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu ambalo lilifungua njia kwa sheria kamili za haki za binadamu.

Liliandikwa na wawakilishi kutoka maeneo yote ya dunia wakiwa na mifumo ya kisheria na kitamaduni tofauti, lilitangazwa na Mkutano Mkuu mnamo 1948. Liliweka wazi , kwa mara ya kwanza, haki za binadamu muhimu kulindwa kote duniani  na limehamasisha katiba za nchi nyingi zilizo huru na demokrasia mpya.

Vita vya Baridi

Wakati wa Vita vya Baridi (mwishoni mwa miaka ya 1940 hadi mapema miaka ya 1990), Umoja wa Mataifa ulifanya kazi muhimu katika kudumisha amani na kudhibiti silaha. Licha ya tishio la vita vya nyuklia, vita vya tatu vya dunia viliepukwa kwa sehemu kubwa kwa sababu ya Umoja wa Mataifa kutoa jukwaa la majadiliano na maamuzi.

Umoja wa Mataifa Leo

Zaidi ya miaka 80 baadaye, Umoja wa Mataifa bado ni shirika kuu la kimataifa, linaloleta usawa na kuratibu hatua za kimataifa katika maeneo kutoka ulinzi wa amani, maendeleo ya kiuchumi hadi biashara.

Wafanyakazi wa UNRWA wanasimamia chanjo ya polio huko Gaza.
© UNRWA
Wafanyakazi wa UNRWA wanasimamia chanjo ya polio huko Gaza.

Mamilioni  ya maisha yameokolewa shukrani kwa msaada wa kibinadamu ulioletwa na Umoja wa Mataifa, ukileta chakula, afya, na makazi katika maeneo ya migogoro na majanga. Mfumo wa Ushirikiano wa kimataifa umeongezeka zaidi  kwa nchi kadhaa na kuhusisha wawakilishi kutoka jamii ya kiraia, vijana, na biashara

Nini Kifuatacho

Nchi Wanachama mara nyingi zinashindwa kukabiliana ipasavyo na vitisho na changamoto za leo za kimataifa, kutoka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na migogoro ya kuvuka mipaka hadi kutokuwepo kwa usawa wa kiuchumi kati ya nchi na ndani ya nchi, na vitisho vya kipevu vya akili bandia isiyodhibitiwa na mabadiliko ya tabianchi.

Ili kuhakikisha kuwa Umoja wa Mataifa unabaki kuwa na uwezo wa kutekeleza jukumu lake kama jukwaa kuu la kimataifa kwa miaka ijayo, mnamo 2020 Nchi Wanachama zilimwalika Katibu Mkuu, António Guterres, kuunda maono ya utawala wa kimataifa bora, kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mapendekezo ya mageuzi katika maeneo kutoka ulinzi wa amani hadi miundombinu ya kifedha ya kimataifa, elimu na ushiriki wa vijana katika utengenezaji wa sera yalifungwa katika Ajenda Yetu ya Pamoja, ambayo ilijumuisha mapendekezo ya kuboresha Umoja wa Mataifa na ambayo baadaye iliingizwa kwenye  mkataba wa kihistoria kwa zama zijazo, iliyopitishwa na viongozi wa dunia katika Mkutano wa Zama Zijazo yaani Summit of The Future katika Umoja wa Mataifa New York, Septemba 2024.

Wito wa Hatua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Katika mwaka wake wa kwanza kama Katibu Mkuu, António Guterres alisema, "kuwa na sheria na mikataba pekee haitoshi." Alihimiza “tunahitaji kujitolea kwa nguvu kwa utaratibu wa kisheria, huku Umoja wa Mataifa ukiwa katikati, na taasisi na mikataba tofauti inayofanya Katiba kuwa hai.” Alitoa wito kwa Ushirikiano wa kimataifa   uliounganishwa  na mashirika mengine ya kimataifa na kikanda  na Ushirikiano wa kimataifa ambayo utastahimili majaribio na vitisho vya leo na kesho.