Baraza la Usalama la UN lakutana kwa dharura kujadili DRC

Baraza la Usalama la UN lakutana kwa dharura kujadili DRC
- M23 wametwaa mji wa Kamanyola jimboni Kivu Kusini
- Tayari wametwaa Goma, Kivu Kaskazini na Bukavu Kivu Kusini
- M23 wameteua viongozi wao akiwemo Gavana na Meya
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mchana wa Jumatano ya Februari 19 wamejulishwa kile ambacho waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wanafanya baada ya kutwaa miji mikuu ya jimbo la Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Akihutubia wajumbe wa Baraza waliokutana kwenye kikao cha dharura kufuatia kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama nchini DRC, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Bintou Keita amesema M23 wameanzisha mamlaka yao.

“Licha ya miito mingi ya kimataifa ya kusitisha mapigano na kukomesha mashambulizi, M23, imeendelea kusonga mbele katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini. Hatua hizi zimekuwa na athari mbaya, zikisababisha kupoteza maisha ya watu wengi wakati M23 walipokuwa wanatwaa udhibiti wa Goma,” amesema Bi. Keita akihutubia wajumbe kwa njia ya video kutoka Kinshasa, mji mkuu wa DRC.
Ameendelea kusema kuwa “katika kipindi cha wiki mbili, Muungano wa Mto Congo, AFC ambao M23 ni moja ya sehemu zake kuu, umeanzisha utawala wake huko Goma kwa kuteua Gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini pamoja na Meya wa mji wa Goma,”
Halikadhalika tarehe 16 Februari, M23 waliteka Uwanja wa ndege wa Kavumu pamoja na mji wa Bukavu ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini.
“Na wameendelea kusonga mbele na jana waliteka mji wa Kamanyola, ambao uko katika eneo linalounganisha mipaka ya nchi tatu ambazo ni DRC, Rwanda, na Burundi,” amesema Bi. Keita ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini, DRC, MONUSCO.
Haki za kibinadamu za wasichana na wanawake zinasiginwa
Bi. Keita amesema mashambulio ya M23 huko jimboni Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yameongeza hatari kwa wasichana na wanawake kukumbwa na ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono unaotokea kwenye maeneo yenye mizozo.

“Watu kulazimika kukimbia, kuongezeka kwa wapiganaji wafungwa na kusambaa kwa silaha kunaongeza hatari hiyo,” amesema.
Kama hiyo haitosho, vikwazo vya kufikisha vifaa vya usaidizi vimeendelea kukwamisha uwezo wa Umoja wa Mataifa kutoa huduma kwa wahitaji.
Amesema wWahudumu wa kibinadamu lazima waendelee kuwa na uwezo wa kufanya kazi zao bila vizuizi ili wasaidie raia walioko hatarini.
Bi. Keita apatia Baraza jukumu
"Ni muhimu kwamba Baraza hili lichukue hatua za haraka na za uamuzi ili kuzuia vita hivi visigeuke na kuwa vya kikanda,” amesema Bi. Keita akiongeza kuwa, “ninatoa wito kwa Baraza hili kuwawajibisha wahusika wa ukiukaji wa haki za binadamu na unyanyasaji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.”
Pongezi kwa hatua ya Baraza la UN la Haki za Binadamu
Amesema katika muktadha huo “ninakaribisha hatua ya tarehe 7 mwezi huu wa Februari ya Baraza la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu ya kupitisha azimio linaloanzisha Tume ya Kusaka Ukweli ambayo itafuatwa na Tume Huru ya uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu huko mashariki mwa DRC.”

Wito kwa pande kinzani DRC
Hatimaye, ametoa wito kwa pande zote kutimiza majukumu yao ya kulinda raia kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu. “Hii ni pamoja na kutoharibu maeneo na vifaa vya Umoja wa Mataifa nchini DRC, ikiwa ni pamoja na usalama wa watu wanaolindwa na MONUSCO.
Matokeo ya kikao cha pamoja cha EAC na SADC
Bi. Keita ametumia hotuba yake pia kuonesha mshikamano na kilichoamuliwa kwenye kikao cha pamoja cha viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC kuhusu hali mashariki mwa DRC kilichofanyika tarehe 8 Februari nchini Tanzania.
“Mkutano huo umesisitiza umuhimu wa kurejelea mazungumzo ya moja kwa moja na majadiliano na pande zote za kiserikali na zisizo za kiserikali, ikiwa ni pamoja na M23, ndani ya michakato ya Luanda na Nairobi,” amesema Bi. Keita, akinukuu ya kwambam mkutano pia umerejelea hitaji la kutokomeza kikundi cha waasi cha FDLR na kuondolewa kwa majeshi ya Rwanda kutoka ardhi ya DRC.
“Ni muhimu kwamba masharti ya tamko la mkutano wa EAC-SADC kuhusu urejeshaji wa huduma muhimu za umma, kufunguliwa kwa uwanja wa ndege wa Goma bila kuchelewa, pamoja na njia kuu za kusambaza umeme, zikiwemo zile za Ziwa Kivu, yatekelezwe mara moja ili kupunguza mateso ya wananchi,” amesema Mkuu huyo wa MONUSCO
Amesema kwa upande wake, Umoja wa Mataifa, ukiwemo MONUSCO, umejizatiti kuunga mkono juhudi zozote zinazolenga kurejesha pande husika kwenye meza ya mazungumzo ili kupata suluhisho la kisiasa la kudumu kwa mgogoro huo, ambao unahatarisha uthabiti wa kanda nzima.
Amesema kwa muktadha huo, “ni muhimu kukumbuka mafanikio makubwa yaliyopatikana katika miezi ya hivi karibuni chini ya mchakato wa Luanda. Ni jambo la msingi, kama ilivyoainishwa kwenye tamko la mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika, AU, uliofanyika Addis Ababa tarehe 14 Februari, kuhakikisha kwamba mafanikio haya hayapotei.
Mjumbe Maalum wa Maziwa Mkuu asema ‘historia inajirudia’
Hivyo ametaja maeneo matatu muhimu ya kuzingatia:
- Kumaliza uhasama kupitia sitisho la haraka la mapigano na pande zote ziheshimu ahadi zao kwenye Mifumo ya Kikanda na Kimataifa ikiwemo ule wa Addis Ababa. Kumaliza ghasia ni suala la dharura ili kuweza kushughulikia mahitaji ya kibinadamu, na kurejesha mazingira rafiki kwa mazungumzo ya kina kuanza.
- Kurejesha mazungumzo akisema jawabu si kupitia jeshi bali mazungumzo ya kisiasa. Mazungumzo na kulegeza msimamo ni ni muhimu ili kufikia suluhisho la kudumu.
- Mfumo wa pamoja wa kikanda wa kutatua mzizi wa mzozo mashariki mwa DRC, kwa kujumuisha mipango ya kati na ya muda mrefu huku wakiendelea kuchechemua Mfumo wa Addis Ababa ili kumaliza kabisa chanzo cha mzozo wa DRC.
Kauli ya DRC
Akizungumza kwa niaba ya mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Waziri wa Mambo ya Nje, Thérèse Kayikwamba Wagner ameeleza mifano ya maelfu ya vifo vya kikatili na majeruhi huko Goma wakati wa mapigano na milipuko ya magonjwa inayotishia maisha ya wengi. Haya, amesema, ni matokeo ya kutekwa kwa Goma na aliloliita kundi la la kigaidi, na kwamba hayo yanafanyika machoni pa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa “ambalo halichukui hatua.”

Wekeni vikwazo kwa makamanda na wanasiasa wa Rwanda
Kauli ya Rwanda
