Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu mambo 5 kuhusu chanjo ya HPV na saratani ya shingo ya kizazi

Mwanafunzi akipatiwa chanjo dhidi ya HPV katika kituo cha afya kusini magharibi mwa Côte d'Ivoire.
© UNICEF/Frank Dejongh
Mwanafunzi akipatiwa chanjo dhidi ya HPV katika kituo cha afya kusini magharibi mwa Côte d'Ivoire.

Fahamu mambo 5 kuhusu chanjo ya HPV na saratani ya shingo ya kizazi

Afya
  • HPV ni kifupi cha Human Papilloma Virus ambayo ni chanjo dhidi ya saratani  ya shingo ya kizazi.
  • Ina nafasi muhimu katika kutokomeza ugonjwa huu unaoathiri mamilioni ya wasichana na wanawake.
  • Katika kila dakika 2, mwanamke mmoja anakufa kutokana na saratani ya shingo ya kizazi.
  • Kuna baadhi ya maeneo idadi ya wagonjwa wapya ni ya juu hadi inatisha

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ulimwenguni, UNICEF kupitia wavuti wake, linasema chanjo dhidi ya virusi vya Human Papilloma au HPV ambavyo ni visababishi vikuu vya saratani ya shingo ya kizazi, inaweza kuzuia asilimia kubwa ya wagonjwa wapya.

Mchanganyiko wa chanjo za HPV na uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi pamoja na matibabu, vina mchango mkubwa katika njia ya kutokomeza ugonjwa huu hatari.

Zaidi ya nchi 130 tayari zimejumuisha chanjo za HPV katika ratiba zao za chanjo za kawaida, lakini hiyo haitoshi. Mamilioni ya wanawake na wasichana, mara nyingi wale wanaoishi katika nchi maskini duniani, hawana wanashindwa kufikia huduma hizo za chanjo, uchunguzi, na matibabu ambayo yanaweza kuokoa maisha yao.

Sasa kuna mambo 5 muhimu unayopaswa kufahamu kuhusu HPV, chanjo, na saratani ya shingo ya kizazi:

1. Saratani ya shingo ya kizazi ni ya 4  kwa saratani zinazokabili wanawake duniani kote.

Mnamo mwaka wa 2022, takriban wanawake 350,000 walikufa kutokana na saratani ya shingo ya kizazi na visa vipya 660,000 vilijitokeza. Vifo na maambukizi haya yanayozuilika yana madhara makubwa kwa watoto, familia, na jamii. Jangwa la Sahara la Afrika, Amerika ya Kati na Kusini-Mashariki mwa Asia vina viwango vya juu vya vifo kutokana na saratani ya shingo ya kizazi.

2.Karibu wagonjwa wengi wenye saratani ya shingo ya kizazi inahusiana na HPV.

Zaidi ya asilimia 95 ya visa vya saratani ya shingo ya kizazi vinatokana na virusi vya human papillomavirus. HPV ni maambukizi ya zinaa (STI) yanayoenea kwa kasi duniani kote. Kuna aina zaidi ya 200 za HPV na nyingi hazioneshi dalili. Hata hivyo, aina za HPV zinazohatarisha zinaweza kusababisha maambukizi sugu na ukuaji wa saratani, ndiyo maana kinga na uchunguzi ni muhimu sana.

Msichana mwenye umri wa miaka 12 nchini Ethiopia anapokea chanjo yake ya HPV ili kujikinga na hatari ya maambukizo ya HPV na saratani zinazohusiana nayo.
© UNICEF/Raphael Pouget
Msichana mwenye umri wa miaka 12 nchini Ethiopia anapokea chanjo yake ya HPV ili kujikinga na hatari ya maambukizo ya HPV na saratani zinazohusiana nayo.

3. Chanjo ya HPV inaweza kuzuia asilimia 90 ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi

Kupata chanjo ni njia bora zaidi ya kuepuka maambukizi ya HPV na inaweza kulinda dhidi ya aina za HPV zinazohusiana na asilimia 90 ya visa vya saratani ya shingo ya kizazi. Nchi nyingi tayari zimeingiza chanjo ya HPV katika programu zao za chanjo za kawaida, hasa kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14. Lakini bado mengi yanahitajika.

4. Uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ni muhimu na yanafaa

Vipimo vya uchunguzi vya mara kwa mara ni njia bora ya kugundua na kutambua saratani ya shingo ya kizazi. Ikiwa inagunduliwa mapema, saratani ya shingo ya kizazi mara nyingi inaweza kuponywa kwa upasuaji pekee. Vifaa vya gharama nafuu na vilivyo na ushahidi kwa uchunguzi na matibabu vinapatikana, lakini hakuna ufikiaji bora wa wanawake na wasichana wengi hawapati huduma hizi kupitia huduma zao za afya za kijamii.

5. Wanawake na wasichana walioko nchi maskini zaidi duniani wako kwenye hatari kubwa.

Saratani ya shingo ya kizazi inaathiri kwa kiasi kikubwa afya na ustawi wa wanawake na wasichana katika nchi za kipato cha chini na cha kati, na inakabiliwa na ukosefu wa usawa duniani kwa ujumla. Kati ya vifo vyote vya saratani ya shingo ya kizazi vinavyokadiriwa mwaka 2022, zaidi ya asilimia 90 vilitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati. Kuongeza upatikanaji wa chanjo nafuu, uchunguzi, na programu za matibabu ni muhimu.

Msichana mwenye umri wa miaka 10 anapokea chanjo yake ya HPV na pepopunda katika jamii ya mashinani nchini Guatemala.
© UNICEF/Sergio Izquierdo
Msichana mwenye umri wa miaka 10 anapokea chanjo yake ya HPV na pepopunda katika jamii ya mashinani nchini Guatemala.

Takwimu za hadi mwaka 2022

  • Chanjo: Chini ya asilimia 25 ya nchi maskini zimejumuisha chanjo ya HPV kwenye ratiba zao za chanjo.
  • Uchunguzi: Chini ya asilimia 5 ya wanawake katika nchi maskini kabisa wamewahi kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi.
  • Matibabu: Chini ya asilimia 5 ya wagonjwa wa saratani wanaoishi katika nchi maskini kabisa wanapata matibabu ya upasuaji salama wa saratani, madhubuti na kwa wakati.

Jinsi UNICEF inavyosaidia

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia  watoto UNICEF, kwa kushirikiana na wahisani na wadau, inafanya kazi kuongeza upatikanaji wa kinga, uchunguzi, na matibabu muhimu ili kufanikisha kumaliza saratani ya shingo ya kizazi kwa:

  • Kutoa chanjo za HPV na vipimo vya uchunguzi kwa nchi ambazo ni nafuu, kwa wakati na vinavyoaminika.
  • Kuimarisha mifumo ya afya ili kuhakikisha kuwa zinaweza kutoa chanjo za HPV kwa ufanisi. Hii inahusisha mafunzo ya wafanyakazi wa afya, kuboresha miundombinu ya afya na kuhakikisha kuwa mifumo ya afya inajiandaa kushughulikia usambazaji wa chanjo.
  • Kufanya kazi kwa karibu na jamii kujenga imani katika programu za chanjo za HPV kwa kushughulikia kutoaminiana kwa chanjo na kuhakikisha kwamba manufaa ya chanjo yanatambuliwa na jamii kwa ujumla.
  • Kuchangia katika utafiti na uzalishaji wa ushahidi kuhusu ufanisi na athari za programu za chanjo za HPV. Hii inajumuisha kukusanya data kuhusu ufanisi  na athari za programu za chanjo kwenye viwango vya saratani ya shingo ya kizazi.