Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yatahadharisha kuhusu tishio la njaa Mashariki mwa DRC  huku watu zaidi wakizikimbia kambi

Wanawake mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini wakibeba chakula kilichowasilishwa na  Umoja wa Mataifa na wadau wake.
WFP
Wanawake mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini wakibeba chakula kilichowasilishwa na Umoja wa Mataifa na wadau wake.

WFP yatahadharisha kuhusu tishio la njaa Mashariki mwa DRC  huku watu zaidi wakizikimbia kambi

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani WFP, limerejelea kwa kiasi usambazaji wa misaada ya chakula katika sehemu za Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), likitoa msaada muhimu wa lishe kwa wastani wa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi miezi 59 waliokumbwa na utapiamlo, huku mapigano ya wiki tatu yakizidi kuathiri vibaya upatikanaji wa chakula kwa wale walio hatarini.

Kulingana na WFP tathmini ya hivi karibuni ya soko imeonesha kuwa bei ya vyakula vya msingi mashariki mwa DRC imepanda kwa kiasi kikubwa na kufanya kuwa vigumu kwa familia kupata chakula. Bei ya unga wa mahindi imepanda kwa karibu asilimia 67, wakati chumvi imepanda kwa karibu asilimia 43, na mafuta ya kupikia yamepanda hadi asilimia 45.

Peter Musoko, Mkurugenzi wa WFP na Mwakilishi wa shirika la WFP nchini DRC amesema, "kadri tunavyoshindwa kutoa chakula na msaada wa dharura kwa familia zinazokumbwa na mzozo, ndivyo mahitaji yao yanavyokuwa mabaya na makubwa. Sitaki kuona watoto na akina mama wakizama zaidi katika njaa na utapiamlo. Tunahitaji vurugu zisimame ili tuweze kurudi katika shughuli zetu za kibinadamu. Watu walio hatarini zaidi nchini DRC hawawezi kupuuziliwa mbali wakati wa janga hili."

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo jijini Kinshasa, DRC inasema kwa njia kuu za kufikia maeneo kufungwa, na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Goma, ambao ni kituo muhimu cha kibinadamu kufungwa, kipaumbele cha WFP ni kurudisha operesheni kikamilifu mara tu itakapokuwa salama kufanya hivyo.

Shirika la ndege la Umoja  wa Mataifa la huduma za kibinadamu UNHAS linaloendeshwa na WFP linahitaji kwa haraka dola milioni 33.1 ili kuendelea na operesheni zake mwaka huu. Bila michango ya ziada, operesheni za anga zinaweza kusitishwa ifikapo mwishoni mwa Machi 2025.

Hapa ni taarifa za hivi karibuni kuhusu operesheni za WFP nchini DRC

• Msaada wa lishe: WFP imesambaza tani 57 za bidhaa za lishe kwenye vituo vya afya ndani ya Goma kusaidia matibabu ya utapiamlo na kufikia watoto 11,000 walio chini ya umri wa miaka mitano wenye utapiamlo, akina mama wajawazito na wanaonyonyesha.

• WFP imerejesha msaada wake kwa kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa Mpox katika maeneo ya Goma, Karusimbi, na Nyiragongo, ikiwaandalia mlo zaidi ya wagonjwa 100 wa Mpox.

•Ghala jipya limeanzishwa Goma ili kuendelea na operesheni za kuokoa maisha. Hii ni baada ya maghala ya WFP kuvamiwa Goma na Bukavu, asilimia 70 ya hifadhi ya chakula ikiibwa Goma, na vifaa vyote vya kibinadamu kutorejeshwa Bukavu.

• Operesheni za UNHAS za WFP zinaendelea kuwezesha ufikiaji wa kibinadamu kwa mikoa ya mashariki. Katika wiki za hivi karibuni, meli za anga zilihamishwa kwenda Kalemie, mkoani Tanganyika, na kuanzisha kituo kipya cha operesheni kwa mashariki mwa DRC.

• Katika mwaka wa 2025, UNHAS imepeleka abiria 2,464, wakiwemo wafanyakazi wa kibinadamu waliohamishwa kutoka Goma na Bukavu, na kuleta tani 23 za mizigo muhimu kote nchini. Operesheni za UNHAS ni muhimu ili kuwezesha na kuweka hali rahisi kwa wafanyakazi wa kibinadamu kufanya kazi muhimu.

• WFP inahitaji dola za Marekani milioni 397 kwa dharura, ili kudumisha operesheni zake za kitaifa kwa miezi sita ijayo