Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufufuaji wa uchumi wa Syria ni muhimu kwa utulivu – Ripoti ya UNDP

Watu milioni mbili wanaishi katika makazi ya muda nchini Syria baada ya kukimbia makazi yao. (Maktaba)
© UNOCHA/Mohanad Zayat
Watu milioni mbili wanaishi katika makazi ya muda nchini Syria baada ya kukimbia makazi yao. (Maktaba)

Ufufuaji wa uchumi wa Syria ni muhimu kwa utulivu – Ripoti ya UNDP

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la  Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) iliyotolewa leo Februarai 20, 2025 inaonya kwamba uchumi wa Syria hautafikia kiwango chake cha kabla ya vita hadi mwaka 2080 kama ukuaji wa kiuchumi hautaongezeka kwa kasi.

Mgogoro wa miaka 14 nchini Syria umefuta mafanikio ya karibu miongo minne ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku Wasyria tisa kati ya kumi wakiishi katika umaskini na mmoja kati ya wanne akiwa hana ajira.

Ili kurejesha uchumi ndani ya muongo mmoja, Syria inahitaji kuongeza ukuaji wake wa kila mwaka mara sita.

Ripoti hiyo, yenye jina Athari za Mgogoro wa Syria, inaangazia madhara makubwa ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na hasara ya Pato la Taifa (GDP) ya dola bilioni 800, uharibifu mkubwa wa miundombinu, na kuenea kwa umaskini. Huduma muhimu kama vile afya, elimu, na nishati zimeporomoka, na kuwaacha mamilioni wakihitaji msaada wa haraka. Zaidi ya asilimia 70 ya mtandao wa umeme umeharibika, huku nusu ya idadi ya watu wakikosa maji safi na huduma za usafi wa mazingira.

Mkuu wa UNDP, Achim Steiner, anasisitiza kuwa zaidi ya msaada wa kibinadamu, Syria inahitaji uwekezaji wa muda mrefu katika ujenzi wa miundombinu, uimarishaji wa kilimo, na urejeshaji wa uzalishaji. Ripoti hiyo inasisitiza kuwa utulivu wa kiuchumi ni muhimu kwa maendeleo endelevu, ikihimiza juhudi za pamoja za kitaasisi na upanuzi wa masoko.

Takwimu muhimu zinaonesha kina cha mgogoro huu: asilimia 75 ya Wasyria wanategemea msaada wa kibinadamu, umaskini uliokithiri umeongezeka mara sita tangu vita vilipoanza, na karibu asilimia 50 ya watoto wa shule hawahudhurii masomo. Kuporomoka kwa mfumo wa afya wa Syria kumechangia vifo na kutoweka kwa mamia ya maelfu ya watu.

UNDP inapendekeza mpango wa urejeshaji uchumi, ikitoa wito wa mageuzi ya utawala, uthabiti wa kiuchumi, na uboreshaji wa huduma za kijamii. Ikiwa Syria itaendelea na kiwango chake cha sasa cha ukuaji wa asilimia 1.3 kwa mwaka, itachukua miaka 55 kufikia urejeshaji kamili wa uchumi. Hata hivyo, kwa kiwango cha ukuaji wa asilimia13.9 kwa mwaka, nchi inaweza kurejea kwenye njia ya maendeleo, na kuweka msingi wa mustakabali thabiti na unaojitegemea.