Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto watota kwa mvua Gaza, huku baridi kali ikitishia afya zao

Wanaume wawili wakishikilia makazi ya hema huku msimu wa hewa ya baridi ukiendelea huko Gaza.
UN News
Wanaume wawili wakishikilia makazi ya hema huku msimu wa hewa ya baridi ukiendelea huko Gaza.

Watoto watota kwa mvua Gaza, huku baridi kali ikitishia afya zao

Msaada wa Kibinadamu

Huko Gaza Kaskazini, kwenye eneo la wapalestina linalokaliwa na Israeli, wanafamilia zilizofurushwa makwao kutokana na vita kati ya Israeli na wanamgambo wa Hamas wanavumilia msimu wa baridi kali katika makazi ya muda ya mahema yanayopigwa na upepo na mvua usiku na mchana, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF. Nyumba zao zimeharibika na kuacha watoto kuishi katika mazingira mabaya. 

Kupitia video iliyoandaliwa na UNICEF, watoto wanaonekana wakitembea katikati ya mahema ya muda kwenye vichochoro vilivvyojubikwa na matope, hapa Gaza Kaskazini, huku wakijaribu kukwepa madimbwi ya maji yaliyosababishwa na mvua kubwa.

Shahd Omar, msichana mwenye umri wa miaka kumi na saba, anaonekana amembeba nduguye, wengine wanaonekana wamekujikunyata kutokana na baridi. Shahd sasa akiwa amesimama nje hema lao anaelezea jinsi nyumba zao zilivyoharibiwa.

Tunavumilia hali ngumu sana,mvua kubwa, baridi, na upepo mkali, maisha ni magumu sana. Nyumba yetu ilivyoshambuliwa na kubomoka tulijitoa kwenye vifusi. Nyumba yetu imeharibika, hatuna samani, hakuna vituo vya kujikinga, wala mahali pa kukaa ili kupata joto. Maisha ni magumu. Hema letu lilikuwa karibu kupeperuka kwa sababu ya upepo mkali.”

Kwingineko hapa, watoto wanaonekana wakicheza kwenye matope nje ya mahema zao huku maji yakitiririka kama mto. Layla Abu Asi ni mama wa watoto watatu, mwenye umri wa miaka 27 anasema,

Baridi hii ni kali mno, haiwezi kuvumilika ,upepo huu mkali umeleta madhara makubwa kwenye hema letu. Tangu asubuhi, maji ya mvua yamejaa kwenye hema letu, kila kitu kilichomo ndani kikilowa na kujaa maji. Watoto wangu wametota kwa maji ya mvua. Hii ni hali mbaya zaidi ambayo tumewahi kukumbana nayo.”

UNICEF na wadau wanafanya kila wawezalo kuwasaidia wakazi wa Gaza.