Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu ya raia zaidi kukimbia DRC, UNHCR yasaka dola milioni 40.4 za kuwasaidia

Maelfu ya watu wamekimbia kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuingia Burundi.
© UNHCR/Bernard Ntwari
Maelfu ya watu wamekimbia kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuingia Burundi.

Hofu ya raia zaidi kukimbia DRC, UNHCR yasaka dola milioni 40.4 za kuwasaidia

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi, UNHCR limetoa ombi la dola milioni 40.4 ili kujiandaa na kutoa huduma za kuokoa maisha na usaidizi kwa wakimbizi wa ndani na waliokimbilia nchi jirani baada ya wakati huu ambapo mashambulizi ya waasi wa M23 yanazidi kufurusha raia

Tweet URL

UNHCR inasema tangu Januari 26 mwaka huu M23 walipoingia Goma, jimboni Kivu Kaskazini, wameendelea na mashambulizi na kutwaa miji sio tu Goma, bali pia Kamanyola na Bukavu jimboni Kivu Kusini.

Fedha hizo zinalenga wakimbizi wa ndani 275,000 walioko majimbo ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini, Manyema na Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, halikadhalika watu wengine 258,000 wanaotarajiwa kukimbia, kusaka hifadhi au kurejea makwao kwenye nchi jirani za Burundi, Rwanda, Tanzania, Uganda na Zambia.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Burundi Brigitte Mukanga-Eno, akizungumzana waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, kwa njia ya video kutoka Bujumbura, amesema tangu Februari, zaidi ya raia 40,000 wa DRC wengi wanawake na watoto wamewasili Burundi kusaka hifadhi ya kimataifa. Idadi hii inaweza kuongezeka kutokana mashambulizi kuelekezwa mji wa Uvira, karibu na mpaka rasmi wa kuingia Burundi.

Na zaidi ya yote “serikali ya Burundi imekuwa na ukarimu mkubwa, na tunashukuru sana kwa kuacha mipaka wazi,  na pia kutangaza utekelezaji wa hatua ya awali ya hadhi ya ukimbizi  kwamba yeyote anayeingia Burundi kusaka usalama, atatambuliwa kuwa ni mkimbizi nchini Burundi.

Bi. Eno amesema lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha wanapata haraka huduma za ulinzi na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Taratibu zinafanyika ili waliokwishawasili Burundi wahamishiwe kwenye kambi ya wakimbizi ya Musenyi iliyoko kusini-magharibi mwa Burundi, kambi ambayo ina uwezo wa kuhifadhi 10,000. Serikali ya Burundi pi aina mpango wa kutenga eneo lingine ili kujenga makazi ya wakimbizi.

UNHCR inasema Uganda imeshapokea wakimbizi 13,000 kutoka DRC, na Tanzania iliripoti kuwa tarehe 19 Februari wakimbizi 53 kutoka DRC waliwasili mkoani Kigoma.

Watu wanaokimbia ghasia mashariki mwa DR Congo eneo la Bukavu, wakisubiri kuvuka mpaka wa Gatumba na kuingia Burundi.
© UNHCR/Bernard Ntwari
Watu wanaokimbia ghasia mashariki mwa DR Congo eneo la Bukavu, wakisubiri kuvuka mpaka wa Gatumba na kuingia Burundi.

Mzigo ni mkubwa kwa Burundi

Bi. Mukanga-Eno amesema mzigo ni mkubwa kwa Burundi kwa sababu hii ni mara ya kwanza Burundi inapokea idadi kubwa ya watu katika muda wa siku chache, kwa kuwa ongezeko la watu lilianza tarehe 14 Februari, na tumeona hasa wiki hii, Jumanne, tulikuwa na watu 9,000 waliovuka mpaka ndani ya siku moja.

Amesema ni wazi kuwa wimbi hili ni kubwa kwa Burundi kupokea katika miaka mingi iliyopita. Kiwango hiki mara ya mwisho ilikuwa miaka ya 2000, kwa hiyo kila mtu amezidiwa uwezo; serikali, lakini vile vile watoa misaada ya kiutu nchini kote.

Mama alibeba watoto wake bila kufahamu wameshafariki dunia

Mwakilishi huyu wa UNHCR nchini Burundi ameelezea simulizi wanazopata kutoka kwa wakimbizi wanaovuka mto Rusizi.

Miongoni mwa visa hivyo ni cha mama mmoja ambaye alikuwa amebeba watoto wake bila kufahamu kuwa tayari walikuwa wamefariki dunia. “Yaani alipofika tu kambini, watoto wake hao wawili walikuwa wamekufa kutokana na uchovu.”

Amesema kuwa watu wanaowasili wako katika hali mbaye, wengi wao watoto, wanawake na wazee. Vijana si wengi. Wanawake na watoto ndio wanaovuka mpaka huu wa mto Rusizi na kuingia Burundi.

Huduma zinaendelea kwa wakimbizi licha ya changamoto

Bi. Mukanga-Eno amesema licha ya changamoto ya huduma kwenye uwanja wa mpira ambako kwa sasa wakimbizi wanaovuka mpaka kupitia mto Rusizi wanahifadhiwa, serikali ya Burundi kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO wameweza kupatia chanjo watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 kufuatia kubainika kwa wagonjwa wawili wa surua wakati wa uchunguzi wa kitabibu.

Lakini vile vile, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeweka huduma ya maboza yam aji. Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP limefikisha msaada wa vyakula ikiwemo vya moto, ingawa mgao ni kiasi kwani watu ni wengi.

Vile vile madaktari wasio na mipaka, MSF nao wameweka kliniki tembezi kuhudumia watu wanaowasili wakiwa wagonjwa.