Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama yatimiza robo karne

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama yatimiza robo karne
Maadhimisho haya yam waka huu ya Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama yanaangazia robo karne ya juhudi za kujitolea kuhifadhi utofauti wa lugha na kuhimiza matumizi ya lugha za mama. Ni fursa muhimu ya kutafakari mafanikio, kurejesha ahadi, na kusisitiza jukumu muhimu la uhifadhi wa lugha katika kulinda urithi wa kitamaduni, kuboresha matokeo ya elimu, na kujenga jamii zenye amani na endelevu, linaeleza shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, (UNESCO).
Wazo la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama lilianzishwa na Bangladesh. Lilipitishwa katika Mkutano Mkuu wa UNESCO mwaka 1999 na limeadhimishwa kote duniani tangu mwaka 2000.
Umuhimu
UNESCO inaamini katika umuhimu wa utofauti wa kitamaduni na lugha kwa jamii endelevu. Ndani ya mamlaka yake ya kuendeleza amani, inafanya kazi kuhifadhi tofauti za kitamaduni na lugha ambazo huimarisha uvumilivu na heshima kwa wengine.
“Jamii za lugha nyingi na tamaduni nyingi huendelezwa kupitia lugha zao ambazo hueneza na kuhifadhi maarifa ya kitamaduni kwa njia endelevu.” Inasisitiza UNESCO na inatahadharisha kwamba, “utofauti wa lugha unazidi kuwa hatarini kadri lugha nyingi zinavyoendelea kutoweka.”
Lugha zinakufa
Kwa mujibu wa UNESCO, duniani kote, asilimia 40 ya watu hawana fursa ya kupata elimu kwa lugha wanayozungumza au kuelewa. Hata hivyo, kuna maendeleo katika elimu ya lugha nyingi, huku kukiwa na uelewa unaoongezeka wa umuhimu wake, hasa katika elimu ya awali, na kujitolea zaidi kwa maendeleo yake katika maisha ya umma.
Kila baada ya wiki mbili, lugha moja hutoweka na hivyo kupotea kwa urithi mzima wa kitamaduni na kiakili. 5
UNESCO inakadiria kuwa duniani kuna lugha 8,324 zinazozungumzwa kwa maneno au kwa njia ya ishara. Kati ya hizi, takriban lugha 7,000 bado zinatumika. Ni lugha chache tu ambazo zimepewa nafasi halisi katika mifumo ya elimu na maeneo ya umma, na chini ya mia moja ndizo zinazotumika katika ulimwengu wa kidijitali.