Wanaokimbia machafuko DRC wasaidiwe kupata hifadhi ya kimataifa - Keita

Wanaokimbia machafuko DRC wasaidiwe kupata hifadhi ya kimataifa - Keita
- Bila shinikizo wachague wanakotaka kuhamia
- Masharti ya M23 kwa MONUSCO yanakwamisha operesheni
- Kampeni za habari potofu na uongo zatishia maisha ya walinda amani
Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakiwa wamekimbilia nchi jirani na wengine wamesaka hifadhi kwenye vituo vya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO kutokana na mashambulizi yanayofanywa na waasi wa M23, hii leo Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini humo ametoa wito wa dharura wa kusaidia raia hao kupata hifadhi.
“Natoa wito wa dharura wa kuwezesha raia wanaokimbia machafuko DRC kuwezeshwa kuhamia nchi mbadala ya chaguo lao, katika mazingira yanayozingatia haki zao, utu na sheria za kimataifa," amesema Bintou Keita, ambaye ni Mkuu pia wa MONUSCO wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kwa njia ya video kutoka Kinshasa, mji mkuu wa DRC.
Amesema anatoa wito huo kwa kuwa jimboni Kivu Kaskazini, tangu M23 watwae mji wa Goma, raia 140,000 wamesaka hifadhi katika vituo vya MONUSCO mjini humo, wakiwemo pia watetezi wa haki za binadamu.
“MONUSCO inajitahidi kutekeleza jukumu lake la ulinzi wa raia licha ya machafuko, lakini hali hiyo si endelevu kutokana na idadi ya waliosaka hifadhi kuwa ni kubwa na huduma ni finyu,” amesema Bi. Keita.
Masharti ya M23 kwa MONUSCO
Bi. Keita amesema kitendo cha baadhi ya maeneo jimboni Kivu Kaskazini kuendelea kushikiliwa na M23 inayoungwa mkono na jeshi la Rwanda, kumekwamisha utekelezaji wa majukumu ya MONUSCO kwenye eneo hilo.
“Mathalani kuna vizuizi barabarani, na MONUSCO inatakiwa kutoa taarifa saa 48 kabla ya jambo lolote inalotaka kufanya, hali inayokwamisha operesheni zake za ulinzi wa raia na usaidizi wa kibinadamu,” amesema Mkuu huyo wa MONUSCO.
Habari potofu na za uongo
Changamoto nyingine ni habari potofu na za uongo pamoja na kauli za chuki dhidi ya MONUSCO.
Amesema vitendo hivyo vimekwamisha operesheni za MONUSCO Kivu Kaskazini na zaidi ya yote kutia hatarini maisha ya walinda amani.
Ingawa hivyo amesema MONUSCO inaendelea kusaidia jeshi la serikali ya DRC, FARDC katika kupeleka vifaa vya matibabu Kivu Kaskazini.
Bi. Keita amezungumzia pia jimboni Ituri ambako amesema ujio wa Kamanda mpya wa MONUSCO umesaidia kuimarisha utendaji wa kazi na kunadhihirisha azma ya kuendelea kutekeleza wajibu.