Uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine umesababisha 'tishio la kisaikolojia', aonya mratibu mkuu wa misaada UN

Uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine umesababisha 'tishio la kisaikolojia', aonya mratibu mkuu wa misaada UN
Katika takriban miaka mitatu tangu uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine, watu wa nchi hiyo wamevumilia mashambulizi ya mara kwa mara, “tishio la kisaikolojia, kufurushwa na mateso", ameonya Afisa wa uratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini humo Matthias Schmale leo Ijumaa, Februari 2025.
Akitoa taarifa akiwa Kyiv, mji mkuu wa Ukraine, baada ya usiku mwingine wa ving'ora vya anga na milipuko mikubwa zaidi ya mabomu, Bwana Schmale amebainisha kuwa mgogoro huo ulianza mwaka 2014 na Urusi kunyakua ‘Crimea’ kinyume cha sheria. "Kwa hiyo, watoto wote hadi walio na umri wa miaka 11 hawajawahi kupata nchi yao ikiwa na amani," amesema.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya dharura OCHA, mwaka wa 2024 ilishuhudia ongezeko la asilimia 30 la vifo vya raia ikilinganishwa na mwaka 2023. "Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya, hasa katika maeneo ya mstari wa vita wa mbele," imesema OCHA katika taarifa, ikionesha kwamba asilimia 36 ya wakazi wa Ukraine ambao ni watu milioni 12.7, wanahitaji misaada ya kibinadamu mwaka huu.
Bwana Schmale anaelezea kuwa "Kuna msukumo mkali sana kutoka kwa vikosi vya kijeshi vya Urusi kwenye mstari wa mbele wa vita hivyo na uokoaji unaendelea. Tunasaidia watu kwa kuwapa bidhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na usaidizi wa fedha, kwa kuwa wanahamia vituo vya muda, maeneo ya pamoja na popote wanapoishi."
UNICEF
Akizungumza kutoka Zaporizhzhia kusini mashariki mwa Ukraine, Toby Fricker, Afisa Mkuu wa mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Ukraine, amesema kuwa zaidi ya watoto 2,520 wameuawa au kujeruhiwa tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi, "idadi halisi inaweza kuwa juu zaidi na hali inazidi kuwa mbaya. Kulikuwa na ongezeko la zaidi ya asilimia 50 la vifo vya watoto mwaka 2024 ikilinganishwa na 2023, na tunachoshuhudia ni kwamba hakuna eneo salama, hakuna shule wala wodi za kinamama wajawazito kujifungulia, hakuna hospitali za watoto, zote zimeathiriwa na mashambulizi." amesema Bwana Fricker.
UN Women
Akisisitiza jukumu muhimu linaloendeshwa na wanawake nchini Ukraine ambalo ni “kubwa kuliko uwanja wa vita”, Mkurugenzi wa ofisi ya Geneva ya shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women, Sofia Calltorp, ameeleza kuwa “kuna hadithi nyingine inayoendelea, na hiyo ni hadithi ya wanawake na wasichana wote wanaobeba mzigo wa vita hii.”
Mnamo mwaka 2024, idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa nchini Ukraine iliongezeka kwa asilimia 30, ameeleza Calltorp akisema, "miongoni mwao, wanawake 800 waliuawa na wanawake zaidi ya 3,700 walijeruhiwa mwaka jana nchini Ukraine. Pia tunajua kuwa sehemu kubwa ya wakimbizi na watu waliotawanywa kutoka Ukraine ni wanawake, na wanawake milioni 6.7 wanahitaji msaada wa kibinadamu wa kuokoa maisha."
Madhara ya Marekani kusimamisha kwa Fedha za ufadhili
Akijibu maswali kuhusu athari za kusimamishwa kwa fedha za Marekani kwa huduma za kibinadamu, Afisa Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine Matthias Schmale, amesema “tumaini kwamba fedha za Marekani zitakuwa sehemu kubwa ya ya mchakato wa ufadhili,” na kuwa mwaka jana, zilichangia asilimia 30 ya kile kilichotumiwa katika upande wa huduma za kibinadamu, na asilimia 10 kwa upande wa maendeleo.
Mkuu huyo wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine amesisitiza kuwa, “kwa hakika tunahofia kuhusu usitishwaji wa uadhili wa marekani, lakini kama tunavyojua sote, bado si mwisho wa siku, kuna mazungumzo mengi yanayoendelea. Tuna baadhi ya wadau wetu, ikiwa ni pamoja na katika Umoja wa Mataifa, ambao wamepata wameanza kupokea ujumbe kutoka marekani kuwa imebadilisha nia, lakini hadi sasa, hakuna pesa zilizotumwa kutokana na misamaha hiyo.”
WHO
Mbali na mashambulizi ya mara kwa mara kwenye miundombinu ya nishati kote Ukraine, vituo vingine vya umma pia vimelengwa, huku vituo vya afya 780 na shule zaidi ya 1,600 vikiharibiwa, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Dunia, (WHO).
"Huko Odessa wiki hii tuliona kliniki ya afya ikitoa huduma kwa watoto 40,000 na shule ya chekechea inayohudumia watoto 250 wenye umri mdogo zaidi iliharibiwa vibaya katika shambulio. Hospitali ya watoto inapopigwa, shule ikilengwa na makombora au gridi ya umeme kuharibiwa, watoto wanateseka hata wakati wanapojaribu kunusurika." amesema Dkt. Jarno Harbicht, Mwakilishi wa WHO nchini Ukraine.
Msongo wa mawazo unaokabili mamilioni ya wakaazi wa Ukraine kwa sababu ya vita unadhoofisha, afisa huyo wa WHO anaendelea akitafakari na kusema, “fikiria mama mchanga katika eneo la Kharkiv nchini Ukraine, siku zake zikikatizwa na ving’ora vya mashambulizi ya anga na usiku wake kuandamwa na droni za vita. Kila siku ni mapambano ya kuchagua kati ya usalama wa watoto wake na kuhimili wasiwasi wao ambao umekuwa wa kawaida kwake.”