Kuelekea miaka mitatu ya uvamizi kamili wa Urusi kwa Ukraine, UN imejiandaa kwa hali zote

Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi ya Ukraine, Matthias Schmale
Kuelekea miaka mitatu ya uvamizi kamili wa Urusi kwa Ukraine, UN imejiandaa kwa hali zote
Amani na Usalama
Shughuli za kidiplomasia zinaongezeka muda mfupi kabla ya kutimia miaka mitatu ya uvamizi kamili wa Urusi kwa Ukraine. Ingawa hali bado ni tete, Umoja wa Mataifa unapanga jinsi bora ya kusaidia Ukraine pindi mapigano yatakapokoma.
Waukraine wanaendelea kukabiliwa na mashambulizi ya kila siku, huku mashambulizi ya anga yakiharibu miundombinu ya raia, na kuwaacha watu bila makazi, joto, au umeme. Zaidi ya watu milioni 10 wamelazimika kukimbia makazi yao, ikifanya hii kuwa mgogoro mbaya zaidi wa uhamaji barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Mapigano yamesababisha vifo vya raia wapatao 12,600 na wengine zaidi ya 29,000 kujeruhiwa. Mashambulizi mengi kwenye vituo vya afya yamewaacha madaktari wakifanya kazi katika mazingira magumu sana. Katika kipindi chote cha mzozo, Umoja wa Mataifa umesaidia usambazaji wa misaada ya kibinadamu, huduma za dharura za matibabu, na urejeshaji wa umeme.
Mustakabali wa Ukraine haujulikani, lakini Umoja wa Mataifa unajiandaa kwa hali mbalimbali za urejeshaji hali nzuri baada ya vita, anasema Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi ya Ukraine, Matthias Schmale, alipofanya mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.
Tunakaribia Makubaliano ya Kusitisha Mapigano
Kiongozi huyo anasema hali ya jumla katika jamii ya kidiplomasia ni kwamba, “tunakaribia kusitisha mapigano, na huenda ikatokea mapema kuliko inavyotarajiwa. Tunajiandaa kwa uwezekano huu kwa kuongeza juhudi za ujenzi na maendeleo.”
Anaendelea kueleza:
Umoja wa Mataifa tayari imefanya kazi kubwa ya kurejesha miundombinu ya nishati iliyoharibiwa, na bila juhudi hizi, wananchi wangekuwa katika hali ngumu zaidi, hasa wakati wa msimu wa baridi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limefungua tena au kurejesha huduma za afya za msingi karibu na mstari wa mbele wa vita, ambazo hapo awali zilifungwa au kuharibiwa. Ikiwa bunduki zitanyamaza, tunaweza kufanya mengi zaidi kusaidia."
Madhara Makubwa kwa Afya ya Akili
"Wadau wetu, wakiwemo serikali, wanaelewa kuwa kanuni ya ‘kutomwacha yeyote nyuma’ inabaki kuwa msingi wa UN. Ndiyo maana tayari tunachambua ni makundi yapi ya watu yatakuwa hatarini zaidi baada ya vita kumalizika.
Miongoni mwa makundi haya ni wanajeshi wa zamani. Nimeambiwa kuna takriban watu milioni moja wanaopigana, wengi wao wakitumia silaha nzito. Mamia ya maelfu watarudi kutoka mstari wa mbele baada ya kuwa mbali na familia zao kwa miaka miwili au mitatu, mara nyingi wakiwa na matatizo makubwa ya kisaikolojia. Hili linaweza kuongeza mvutano wa kijamii, ikiwa ni pamoja na ongezeko la ukatili wa kijinsia.
Nchi itaendelea kukumbwa na athari za vita hivi kwa muda mrefu, hasa katika eneo la afya ya akili. Mfumo wa Umoja wa Mataifa tayari unatoa msaada katika eneo hili. Kwa mfano, shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) limeunda programu maalumu ya kidijitali kwa ajili ya wanajeshi wa zamani kupata huduma wanazohitaji. “Pia tumeanzisha zaidi ya ‘maeneo salama’ 80 ambako makundi yaliyo hatarini, kama vile watoto waliokimbia makazi yao na wanawake waliokumbwa na ukatili wa kijinsia, wanaweza kushiriki uzoefu wao na kupata msaada wa kisaikolojia.”
Kuna pia mjadala mkubwa kuhusu uwezekano wa wakimbizi kurejea nyumbani. Miezi michache iliyopita, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kwa kushirikiana na serikali ya Ukraine, lilizindua tovuti inayotoa taarifa kwa wakimbizi walioko nje ya nchi kuhusu huduma zinazopatikana wanaporejea, ikiwa ni pamoja na msaada wa makazi na ajira. Tunajiandaa kupanua kwa kiasi kikubwa juhudi hizi.
Kujiandaa kwa Hali Yoyote
Swali kuu linalosalia wazi ni aina gani ya makubaliano ya kusitisha mapigano yatakayofikiwa, hasa katika maeneo yanayokaliwa mashariki na kusini mwa Ukraine. Takriban Waukraine milioni moja wanaishi katika maeneo haya, na bado haijulikani ni nini kitawapata. Je, eneo la kutokuwa na silaha litaanzishwa? Je, kikosi cha kulinda amani cha kimataifa kitahakikisha usitishaji mapigano? Je, ni fursa gani zitafunguka kwa misaada ya kibinadamu?
Kwa upande mwingine, ingawa kila mtu anatumai kusitishwa kwa mapigano, kuna uwezekano pia wa hali mbaya zaidi. Kuna vinu kadhaa ya nyuklia nchini Ukraine, na kama moja yao itashambuliwa, tunaweza kukumbwa na janga kubwa la nyuklia. Hili linazua wasiwasi mkubwa miongoni mwa mamlaka za nchi. [Mnamo Februari 15, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) liliripoti kuwa shambulio la ‘droni’ au ndege zisizo na rubani lilisababisha tundu kwenye muundo wa ulinzi wa mtambo wa nyuklia wa Chernobyl. Licha ya uharibifu mkubwa, viwango vya mionzi havikubadilika.]
“Bila kujali jinsi hali itakavyobadilika, tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba Umoja wa Mataifa inabaki tayari kwa hali yoyote inayoweza kutokea." Anaahidi Matthias Schmale.