Baraza la Usalama la UN yaitaka Rwanda iache kusaidia waasi wa M23 nchini DRC

Baraza la Usalama la UN yaitaka Rwanda iache kusaidia waasi wa M23 nchini DRC
- Rwanda yatakiwa iache kusaidia M23
- Yatakiwa pia iondoe jeshi lake DRC
- Rwanda na DRC zianze mazungumzo ya kidiplomasia bila masharti yoyote
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wajumbe 15, kwa pamoja wamepitisha azimio Ijumaa Februari 21, likilaani vikali mashambulio yanayoendelea kufanywa na waasi wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Wajumbe wote 15 wamepitisha azimio
Katika kikao chao kilichofanyika jioni ya Ijumaa, wajumbe hao wakiwemo wa kudumu, Marekani, Ufaransa, Uingereza, Urusi na China wameitaka jeshi la Rwanda liache mara moja kusaidia kundi hilo la waasi na liondoke kutoka eneo la DRC bila masharti yoyote.
Wajumbe wengine 10 wasio wa kudumu kwenye Baraza hilo ni Somalia, Sierra Leone, Algeria, Pakistani, Guyana, Korea Kusini, Panama, Slovenia, Denmark na Ugiriki.
Baraza pia kupitia azimio hilo namba 2773 la mwaka (2025 wamesisitiza wito wa dharura kwa pande kinzani kukamilisha haraka sitisho la mapigano bila masharti yoyote, kama ilivyotakiwa kupitia mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC.
Halikadhalika wamesihi DRC na Rwanda “bila masharti yoyote zirejee kwenye mazungumzo ya kidiplomasia kama suala la dharura ili kufanikisha amani ya kudumu kwenye mzozo huo wa muda mrefu katika Ukanda huo wa Maziwa Makuu Afrika.”
Ujumbe ulio dhahiri
Azimio hilo liliwasilishwa na Ufaransa ambaye Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Nicolas de Rivière, ameshukuhuru wajumbe wa Baraza kwa azma yao wakati wa mashauriano katika kipindi cha wiki nzima iliyopita.
“Azimio linatuma ujumbe wa wazi” hakuna suluhu ya kijeshi kwenye mzozo wa DRC,” amesema, na kuongeza kuwa shambulio la M23 linaloungwa mkono na Rwanda lazima likome.
Hali ya usalama Mashariki mwa DRC imeendelea kuzorota tangu Januari baada ya waasi wa M23 kusonga kwenye majimbo ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini, huku janga hilo likisambaa sasa katika jimbo la Ituri.
Waasi hao wametwaa mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma na ule wa Kivu Kusini, Bukavu, huku maelfu ya watu wakiripotiwa kuuawa, na hata kufurushwa makwao, ikiwemo kukimbilia nchi jirani.
Ruhusu misaada kufikia wahitaji
Azimio hilo pia linalaani vikali mashambulizi yoyote dhidi ya raia na miundombinu, ikiwemo ile ya Umoja wa Mataifa, wahudumu wa kiutu na wahudumu wa afya.
Halikadhalika linalaani mauaji holela ya raia, kukata watu viungo, ukatili wa kingono na wa kijinsia, usafirishaji haramu wa binadamu na utumikishaji vitani wa watoto.
Baraza limetaka pande zote kuruhusu ufikishaji salama na haráka na bila vikwazo vyovyote wa misaada ya kiutu, na kurejesha huduma za msingi kama vile afya maji, umeme na mawasiliano.
Baraza limesisitiza mshikamano wake na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini, DRC, MONUSCO, na kusisitiza kuwa mashambulio yoyote dhidi ya walinda amani, yanaweza kuwa uhalifu wa kivita.